Rozari Takatifu (Matendo ya Uchungu) - Jumanne na Ijumaa
1. Yesu Anatoka Jasho la Damu
Akasema, "Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe." (Marko 14:36)
Ee Bwana, tunakuomba usitutie katika majaribu, bali utujalie nguvu ya kuvishinda vishawishi vyote. Tunawaombea wadhaifu, wagonjwa na wanaoteseka, ili uwape nguvu ya kufanya mapenzi yako.
2. Yesu Anapigwa Mijeledi
Pilato akawaambia, "kwani ni ubaya gani alioutenda?" Wakazidi sana kupiga kelele, "Msulubishe!" Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulubiwe. (Marko 15:14-15)
Ee Bwana, wakati tunapokosewa haki, tunapodharauliwa na kutendewa ubaya bila sababu, tusaidie kuyakumbuka mateso yako. Tunawaombea haki wote wanaonyanyaswa, waliofungwa na wanaoteswa kwa ajili ya imani zao za kidini, kijamii na kisiasa.
3. Yesu Anavikwa Taji la Miiba
Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndio Praitorio (yaani nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamtia kichwani. (Marko 15:16-17)
Ee Bwana, tunakuomba uondoe mioyo yetu hisia zote za chuki na kulipiza kisasi. Tufanye tuwapende na kuwasamehe wote wanaotupa uchungu.
Tunakuomba utujalie roho ya upatanisho wanandoa waliotalakiana, familia zinazogombana, jamii na makabila yanayobaguliwa, na mataifa yanayopigana.
4. Yesu Anaubeba Msalaba Wake
Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulubiwe; nao wakampokea Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. (Yohana 19:16-18)
Ee Bwana, tujalie neema ya kudumu na kuwa waaminifu mpaka mwisho. Tunawaombea wakosefu wote waliokuasi. Tupatie sote neema ya kutubu, ili tuweze kuubeba msalaba wetu na kumfuata mwanao.
5. Yesu Anakufa Msalabani
Basi alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, "Imekwisha." Akainama kichwa, akaisalimu roho yake. (Yohana 19:30)
Ee Bwana, kwa maombezi ya mama yako mtakatifu, aliyesimama chini ya msalaba, tunakuomba uwe nasi sasa, na hasa saa ya kufa kwetu. Kwa njia ya kipekee tunawaombea wote wanaokufa, ili waweze kufika Mbinguni.