Rozari Takatifu (Matendo ya Mwanga) - Alhamisi
1. Ubatizo wa Yesu Mtoni Yordani
Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka Mbinguni ikisema, "Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye." (Mathayo 3:13, 16-17)
Ee Mungu, kwa fadhili zako, kwa maji na Roho Mtakatifu, tunazaliwa katika maisha ya uzima wa milele. Tunakusihi kwa wema wako uendelee kuzimimina baraka zako juu yetu; na kutufanya kuwa wana waaminifu wa taifa lako takatifu. Amina.
2. Yesu Ageuza Maji Kuwa Divai Huko Kana
Na siku ya tatu palikuwa na harusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, "Hawana divai." Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, alimwita bwana harusi, akamwambia, kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta ilio dhaifu; wewe umeiweka divai ilio njema hata sasa.
Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. (Yohana 2:1-3, 9-11)
"Ee Bwana, tunakuomba ujalie ili upendo ukiimarishwa na neema ya sakramenti ya ndoa, uweze kushinda udhaifu na majaribu yote yanayozikumba familia zetu wakati mwingine. Kwa maombezi ya familia takatifu ya Nazareti, lijalie Kanisa liweze kutekeleza utume wake kwa fanaka duniani kote ndani ya familia na kwa ajili ya familia. Amina." (Papa Yohana Paulo wa pili)
3. Yesu Atangaza Ufalme wa Mungu
Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri habari njema ya Mungu, akisema, "Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini injili." (Marko 1:14-15)
Tuwaombee watu wote, wanaume kwa wanawake, wa kila kabila na taifa, ili wamtambue Mungu mmoja, aliye Baba wa wote, na kwa mshikamano wa undugu waweze kuutafuta ufalme wake ambao ni amani na furaha katika Roho Mtakatifu. Amina.
4. Kugeuka Sura Kwa Yesu
Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, "Huyu ni mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye." (Luka 9:28-35)
Ee Bwana, tunakuomba uinue nyoyo zetu juu ya udanganyifu wa vitu tuvionavyo, uoga na uvivu, ubinafsi na uchoyo, mila na mitindo na kuzituliza kwenye ukweli wako wa milele, ili tuweze kuishi kwa furaha na uhuru tukitumaini kwa imani kwamba u mwokozi wetu, mfano na rafiki yetu, hapa duniani na katika uzima ujao. Amina
5. Kuwekwa Kwa Ekaristi
Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, "Twaeni; huu ndio mwili wangu." Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, "Hii ndio damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi: Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu." (Marko 14:22-25)
"Upende kutufanya, Ee Bwana, tustahili kuwatumikia ndugu zetu, wanaume kwa wanawake, duniani kote ambao wanaishi na kufa katika umaskini na njaa. Wapatie kwa njia ya mikono yetu leo hii mkate wao wa kila siku, na kwa upendo wetu, wajalie amani na furaha." (Mama Teresa wa Calcutta)