Rozari Takatifu (Matendo ya Furaha) - Jumatatu na Jumamosi
1. Malaika Anampasha Habari Maria Kwamba Atakuwa Mama wa Mkombozi
Malaika akamwambia, "Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema; na jina lake utamwita Yesu... Mariamu akasema, "Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema."
Ee Bwana, tujalie imani ukubali mapenzi yako daima bila kusitasita. Tunawaombea pia wale wote ambao hawakujui, lakini wanakutafuta kwa moyo mnyofu.
2. Bikira Maria Anakwenda Kumtembelea Elisabeti
Basi Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu. (Luka 1:39-41)
Ee Bwana, ijaze mioyo yetu furaha na shukrani kwa kuwa umetuita kuwa watoto wako. Kwa njia ya pekee tunawaombea wakatekumeni na wale wote ambao kwa mafundisho yao, wanawaongoza kwako.
3. Yesu Anazaliwa Bethlehemu
Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. (Luka 2:6-7)
Ee Bwana, amani yako na ibaki mioyoni mwetu daima tunapojaribu kukupendeza na kuishi kwa ajili ya utukufu wako. Tunaiombea nchi yetu, wote wenye madaraka na watumishi wa uma, ili waweze kufanya kazi kwa amani na haki, na kwa manufaa ya wote.
4. Yesu Anatolewa Hekaluni
Kisha zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, "Kila mtoto mwanaume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana." (Luka 2:22-23)
Ee Bwana, tusaidie tuyatolee maisha yetu yote kwako, mwili na roho, kazi na mapumziko, furaha na uchungu. Tunawaombea pia mapadre wetu ili kwa njia ya sala zao, mahubiri na njia ya maisha waweze kutuongoza kwako.
5. Maria na Yusufu Wanamkuta Yesu Hekaluni
Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, "Mwanangu, mbona umetutenda hivi?" Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, "Kwani kunitafuta? Hamkujua imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?" (Luka 2:48-49)
Ee Bwana, tufundishe kuheshimiana na kuchukuliana kwa upendo, kwa sababu unaishi ndani yetu. Tunaziombea familia zetu na familia zote, ili wazazi na watoto waishi katika upendo na kuheshimiana.